JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
BUNGE
LA TANZANIA
________________
TAARIFA YA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI KUHUSU
UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI KWA MWAKA WA FEDHA
2015/2016 PAMOJA NA MAONI YA KAMATI KUHUSU
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA
WA FEDHA 2016/2017
_______________
MEI, 2016
TAARIFA YA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI KUHUSU UTEKELEZAJI
WA MAJUKUMU YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI KWA MWAKA WA FEDHA 2015/2016 PAMOJA
NA MAONI YA KAMATIKUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA
MWAKA WA FEDHA 2016/2017
________________________
1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya
99 (9) na Kanuni ya 117(11), ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016, naomba kuwasilisha
Taarifa ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, kuhusu utekelezaji
wa majukumu ya Wizara ya Nishati na Madini kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016,
pamoja na Maoni ya Kamati kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha
2016 /2017.
Mheshimiwa Spika, Kamati ilikutana kwa lengo la kupokea
na kuchambua Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha
2015/2016 na kupitia Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Spika, Katika kufanikisha jukumu hili, Kamati ili tekeleza shughuli zifuatazo:-
i) Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo iliyoidhinishiwa Fedha
kwa mujibu wa Kanuni ya 98(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari,
2016.
ii) Mapitio ya Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka
wa Fedha 2015/2016 kwa mujibu wa Kanuni ya 98(2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge.
iii) Uchambuzi wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara
hii kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Spika, Taarifa hii inaonesha matokeo ya shughuli hizo pamoja na Maoni na
Ushauri wa Kamati kwa mujibu wa Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge.
2.0 UKAGUZI WA MIRADI YA MAENDELEO ILIYOTENGEWA FEDHA KWA MWAKA 2015/2016
Mheshimiwa Spika, Kamati ilizingatia masharti ya Kanuni ya 98(1) ya Kanuni za Kudumu za
Bunge Toleo la Januari, 2016 kwa kutembelea Mikoa ya Dar Es salaam, Mtwara, Manyara,
Njombe na Mbeya kwa lengo la kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya
maendeleo chini ya Wizara ya Nishati na Madini iliyotengewa na kupelekewa Fedha
kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016. Naomba kulijulisha Bunge lako Tukufu kuhusu
miradi hiyo kama ifuatavyo:-
i) Kinyerezi
I MW 150.
ii) Bomba
la Gesi Mtwara
iii) Mgodi wa Tanzanite one,
iv) Makambako/Songea
Transimission Line wenye msongo wa kilovoti
220
v) REA
katika vijiji vya mkoa wa Njombe pamoja
na
vi) Mgodi
wa Makaa ya Mawe Kiwira.
2.1
Maelezo kuhusu Miradi ya Maendeleo
iliyokaguliwa
Mheshimiwa Spika, Miradi iliyokaguliwa
na Kamati kwa ujumla wake inahusu mambo muhimu yafuatayo;
i)
Uzalishaji wa Umeme
wa Kinyerezi I MW 150;
ii)
Bomba la kusafirisha
gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam pamoja na mitambo ya kuchakata na
kusafisha gesi ya Mnazi bay na Songo Songo;
iii)
Mradi wa
Makambako/Songea wa kusambaza umeme katika mikoa ya Ruvuma na
Njombe. Kamati ilikagua utekelezaji wa mradi katika vijiji vya Lyamkena,
Itipingi, Igongolo na Tagamenda;
iv)
Mradi wa REA katika Mkoa
wa Njombe. Kamati ilikagua utekelezaji wa mradi huo katika vijiji vya
Itulahumba, Isindangosi, Iteni, Usuka, Mlevela pamoja na Nyumbanitu na Kichiwa;
v)
Mgodi wa Tanzanite
One;
vi)
Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira;
2.2
Matokeo ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kwa Mwaka
wa Fedha 2015/2016
2.2.1
Miradi ya Sekta ya Nishati
2.2.1.1
Mradi wa REA
Mheshimiwa Spika, Miradi ya REA inagharamiwa na fedha za Mfuko wa Nishati
Vijijini ambao vyanzo vyake vya Mapato ni pamoja na tozo ya shilingi 100 katika kila lita ya mafuta
ya Petroli na Dizeli na shilingi 150 katika kila lita ya mafuta ya taa.
Kamati inasikitishwa na hali ya kusua sua katika upelekaji wa fedha za miradi ya REA, licha ya
fedha hizo kuwekewa wigo wa kisheria( Ring fenced).
Takwimu
zinaonesha kwamba tangu Tozo hizi ilipoanza kukusanywa Julai 2013 hadi kufikia
Machi, 2016 jumla ya shilingi Bilioni 493.8 zimekusanywa kutoka kwenye tozo za
Petroli na Dizeli, shilingi bilioni 448.5 kutoka kwenye Mafuta ya Taa na shilingi
bilioni 45.4 kutoka kwenye Custom Processing Fee.
Mheshimiwa Spika, licha ya makusanyo
hayo, kiasi cha fedha kilichopelekwa kwenye Mfuko wa Nishati Vijijini hadi
Aprili 2016 ni shilingi bilioni 366.95 s.awa na asilimia 37.15 ya makusanyo
yote kutoka kwenye Tozo hizo.
Aidha,
Kamati hairidhishwi na mwenendo wa utolewaji wa fedha za bajeti
zinazoidhinishwa kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya REA. Takwimu zinaonesha kwamba, katika miaka mitatu
ya fedha iliyopita (2013/14 hadi Aprili 2015/16 wastani wa upatikanaji wa fedha
za REA ulikuwa ni kwa asilimia 60. Ufafanuzi kuhusu mwenendo wa upatikanaji wa
fedha kwa kipindi cha miaka mitatu umeelezwa katika jendwali lifuatalo:-
Mwaka wa Fedha
|
Fedha iliyoidhinishwa
|
Fedha iliyotolewa
|
Asilimia ya Lengo
|
2013/2014
|
Bilioni 285.5
|
BIlioni 184.9
|
65
|
2014/2015
|
Bilioni 271.6
|
Bilioni 189.7
|
70
|
2015/2016
|
Bilioni 357.1
|
Bilioni 168.9
Hadi Aprili 2016
|
47.3
|
Mheshimiwa Spika, Kamati inahoji juu ya wapi zilipo shilingi bilioni 73.5 ambazo ni
tofauti ya tozo zilizokusanywa na Mfuko wa Nishati Vijijini katika kipindi cha
miaka mitatu ikilinganishwa na bajeti iliyoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya
kutekeleza Miradi ya REA? Kutojulikana zilipo fedha hizo kuna leta hisia kwa
Kamati kwamba fedha hizi zina matumizi mengine tofauti na yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika, Kamati inalishauri
Bunge lako liitake Serikali itoe ufafanuzi wa kina ni kwanini fedha hizi ambazo
ukusanyaji wake ni wa uhakika na zimewekewa wigo kisheria (Ring fenced)
hazipelekwi kwenye utekelezaji wa miradi REA? Vinginevyo Kamati haioni
mantiki ya kuweka tozo kwenye mafuta nakuendelea kumuumiza wanachi ilihali
fedha hizo hazitekelezi jambo lilokusudiwa.
Mheshimiwa Spika, kutotolewa kwa fedha
za REA kikamilifu kumekuwa na athari mbalimbali katika usambazaji wa umeme
vijijini, ikiwa ni pamoja na Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya REA kutolipwa
kwa wakati jambo linaloongeza gharama za mradi. Aidha, utaratibu
unaidhihirishia Kamati kuwa, Wizara haitaweza kufikia malengo ya kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa Sekta ya
Nishati kwa maendeleo endelevu ya Taifa.
Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine ni
TANESCO kushindwa kushindwa kusimamia kikamilifu Wakandarasi wanao tekeleza miradi na hivyo kusababisha miradi
hiyo kutekelezwa chini ya kiwango. Kwa mfano katika mkoa wa Njombe Wakandarasi
walifunga mashine Humba (Transformers) 60 zilizochini ya kiwango hadi
wakati Kamati inafanya ziara mashine 35 kati ya hizo zilikuwa zimeisharibika.
2.2.1.2
Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira
Mheshimiwa Spika, iwapo Mgodi wa Makaa
ya Mawe Kiwira utaanza uzalishaji, utaongeza umeme kwa MW400. Uzalishaji huu
utaboresha upatikanaji wa umeme na kuchangia kufikiwa kwa azma ya nchi yetu kuingia katika uchumi
wa Viwanda. Hata hivyo, kamati inasikitishwa kuwa haioni dhamira ya dhati ya
Serikali kuendeleza Mgodi huu kutokana na sababu zifuatazo:-
Moja, kiasi cha fedha ambacho
kimekuwa kikitengwa kwa ajili ya mgodi huu ni kidogo sana na kisicho zingatia
mahitaji ya Mgodi, Kwa mfano kiasi cha fedha kinachohitajika ili mgodi uweze
kuanza uzalishaji wa MW 50 kwa awamu ya kwanza unahitaji jumla ya shilingi
bilioni 145 lakini katika mwaka wa fedha
2015/2016 mgodi uliidhinishiwa
shilingi Bilioni 2 tu. Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017 mgodi
umetengewa kiasi kile kile.
Mbili, kutopelekwa kwa fedha
zinazoidhinishwa. Kamati imebaini kwamba, licha ya fedha zinazoidhinishwa kwa
ajili ya mgodi kuwa ni kidogo fedha hizo hazipelekwi. Kati ya shilingi bilioni
2 zilizoidhinishwa katika mwaka wa fedha 2015/2016 hakuna fedha yoyote
iliyopelekwa hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Aprili 2016.
Tatu,
Serikali kutokuwa na mkakati wa kupata matumizi mengine ya madini haya,
kunalipunguzia Taifa pato kubwa ambalo lingeweza kupatikana kupitia Makaa ya
mawe. Kamati inaishauri Serikali kufanya mazungumzo na Viwanda vya simenti ili
vitumie makaa ya Mawe yanayozalishwa hapa nchini. Mfano:- Kiwanda cha DANGOTE
kinatumia Makaa ya Mawe kutoka Afrika Kusini.
Mheshimiwa Spika, Kamati inashauri
Serikali kuwa kama haijawa na dhamira ya dhati ya kuanzisha uzalishaji katika
Mgodi huu ni vema Bajeti kidogo inayotengwa ikaelekezwa katika Miradi mingine
ya Nishati.
2.2.1.3 Mradi wa njia ya
kusafirishia umeme wa msongo wa kilovoti 220 wa Makambako/Songea
Mheshimiwa Spika, Mradi huu unaotekelezwa kwa ufadhili kwa pamoja baina ya
Serikali ya Swedeni na Tanzania, unahusisha ujenzi wa njia ya umeme ya msongo
wa kilovolti 220 yenye urefu wa kilometa 250 kutoka Makambako hadi Songea,
ambayo inatarajiwa kuwa na uwezo wa kusafirisha (carrying capacity) MW 150 za nishati ya umeme. Aidha, mradi huu
muhimu kwa mikoa ya Njombe na Ruvuma
umeshindwa kukamilika kwa wakati kutokana changamoto ya upatikanaji
wa fedha za kulipa Wakandarasi.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, hatua
ya Kamati yako kufanya ziara ya ukaguzi imesaidia
mradi huo kupelekewa fedha zilizokuwa
zimekwamba kutoka Hazina. Hali hii inadhihirisha kwamba fedha ya mradi
ilikuwepo lakini hakuwa na dhamira ya kuipeleka.
Utaratibu
huu wa kuchelewesha fedha za miradi umekuwa ukiingizia Serikali hasara kwani
imekuwa ikilazimika kulipa fidia kwa Wakandarasi kutokana na kuchelewesha
malipo.
2.2.2
Miradi
Sekta ya Madini
2.2.2.1 Madini ya Vito
2.2.2.1.1 Madini ya Tanzanite
Mheshimiwa Spika,
Tanzanite ni madini yanayopatikana Tanzania peke yake, hata hivyo kama Taifa
tumekuwa hatunufaiki na mapato yanayotokana na uchimbaji wake, kutokana na
Serikali kukosa mfumo madhubuti wa usimamizi.
Vilevile,
kukosekana kwa miundombinu ya kukata Tanzanite hapa
nchini kumesababisha Wawekezaji pamoja na wachimbaji wadogo wadogo kutorosha
madini nje ya nchi kwa kigezo cha kwenda kuyasafisha. Jambo
hili siyo tu kwamba lina ikosesha nchi mapato stahiki, bali linatufedhehesha
kama Taifa pekee linalozalisha madini haya dunia kwa kutufanya tushike nafasi ya nne nyuma ya
nchi za India, Afrika Kusini na Kenya katika uuzaji wa Tanzanite.
Mheshimiwa Spika,
kwa kuwa hakuna dhamira ya dhati ya Serikali ya kudhibiti utoroshaji wa
Tanzanite ghafi, kamati inashauri kuwa
usimamizi wa Mgodi huu uangaliwe upya ili kulinda rasilimali hii muhimu.
Mheshimiwa Spika,
Kamati inasikitishwa na jitihada finyu za kutafutia ufumbuzi wa mgogoro wa muda
mrefu kati ya Wachimbaji wadogo na mwekezaji. Mgogoro huu unatokana na
muingiliano wa maeneo ya uchimbaji chini ya ardhi (maarufu kama “mitobozano”).
Pia Sheria ya madini inachangia ukuaji wa mgogoro huu kwa kukosa vifungu
vinavyoelezea uchimbaji wa madini ya Tanzanite, ambao ni tofauti ikilinganishwa
na uchimbaji wa madini mengine.
Serikali
imeunda
Tume zaidi ya 6 kati ya mwaka
2002 hadi 2008 kwa lengo la kutafuta
ufumbuzi wa mgogoro baina ya Wawekezaji na Wachimbaji wadogo wadogo. Hata
hivyo, Maoni na ushauri wa Tume hizi haujafanyiwa kazi jambo linalisababisha
kuendelea kukua kwa mgogoro huo.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa
juhudi za Serikali katika kushughulikia mgogoro huu zimeonekana kushindwa,
Kamati inalishauri Bunge lako tukufu lifuatilie kwa kina mgogoro huu kwa
maslahi ya Taifa letu.
2.2.2.1.2 Madini ya Almasi
Mheshimiwa Spika,
pamoja na uchimbaji wa muda mrefu wa Almasi hapa nchini, Taifa limekuwa halinufaiki
na mapato yatokanayo na rasilimali hii. Mgodi pekee unaochimba madini hayo wa
Mwadui umekuwa haulipi Corporate Tax kama inavyotakiwa kisheria kwa kisingizio
cha kuzalisha kwa hasara.
Kwa mujibu wa takwimu za
Mamlaka ya Mapato Tanzania, mgodi huu umelipa kodi ya mapato (corporate tax)
kwa miaka minne tu ambayo ni kuanzia mwaka 2008/2009 hadi 2013/2014.
Mheshimiwa
Spika, Kamati haiamini kwamba mgodi huu umekuwa
ukijiendesha kwa hasara kwa miaka yote ambayo umekuwa ukifanya shughuli za
uchimbaji wa madini hayo kama unavyodai. Iwapo
madai hayo yangekuwa na ukweli wowote, ni wazi kwamba mgodi ungekuwa umeshafunga shughuli za uzalishaji.
2.2.2.2 Madini ya Dhahabu
Mheshimiwa Spika, uchambuzi
wa Kamati umebaini kuwa migodi
mikubwa ya dhahabu nchini hailipi kodi ya mapato (Corporate tax) kwa kisingizio
cha kupata hasara endelevu katika uzalishaji.
Hata hivyo kamati haikubaliani na
sababu hiyo kwani taarifa zinaonesha kwamba makapuni yanayomiliki migodi hiyo
yamekuwa yakipata faida kwenye masoko ya hisa ambako kampuni hizi zimesajiliwa.
Aidha,
Ripoti ya TMAA ya mwaka 2015 inaonesha kwamba makapuni ya madini ya dhahabu
hayakulipa jumla ya shilingi bilioni 10.27 kwaajili ya ushuru wa Huduma (Service
Levy), na Mrabaha (Royalty) kwenye Halmashauri husika. Kamati inaitaka Serikali ifuatilie malipo ya tozo hizo.
Mheshimiwa Spika, Kamati
inasikitishwa na ulipaji mbovu wa
kodi kwa mgodi wa ACACIA (zamani Baarick gold na African Barrick Gold) kwa kutolipa kodi ya zuio (Withholding Tax) na kodi ya mapato(Corporate Tax) kwa miaka
minne hata baada ya kuamriwa na mahakama ya usuluhishi kulipa kodi hiyo inayofikia jumla ya shilingi
bilioni 89.
Kamati
inaitaka Serikali kuchukua hatua madhubutu
juu ya mwenendo huo. Ili iweze kudhibiti
ukosefu wa mapato kama ilivyotokea kwenye migodi ya Resoulte na Tulawaka ambayo
ilifunga shughuli za uchimbaji bila kulipa kodi stahiki.
Mheshimiwa Spika,
kamati inatambua jitihada ambazo zimekuwa zikifanywa na Serikali katika
kuwawezesha Wachimbaji wadogo wadogo katika shughuli zao za uchimbaji kwa
kuwatengea maeneo ya uchimbaji, kuwapa ruzuku na kuwajengea uwezo kupita mafunzo
mabalimbali. Hata hivyo, jitihada hizi bado hazijakidhi mahitaji kwani kumekuwa
na malalamiko ya Wachimbaji wadogo wadogo kukosa maeneo ya uchambaji pamoja na
mitaji.
Pia
Wananchi wa maeneo yanayozunguka migodi waliochukuliwa maeneo yao wamekuwa
wakilalamika juu ya kucheleweshewa au kutolipwa fidia zao. Mfano mzuri ni wananchi wa maeneo ya Nyamongo na Nyamichele yanayozunguka mgodi wa North Mara ambao maeneo
yamechukuliwa na Mgodi zaidi ya miaka mitatu iliyopita lakini hawajalipwa faidi
hali hii inawafanya wananchi hawa kuishi maisha ya shida na kushindwa
kuendeleze shughuli zao mbalimbali.
2.3
Miradi
ya Gesi.
Mheshimiwa Spika, Sekta ya gesi
asilia ina fursa kubwa ya kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. Hata hivyo
ugunduzi wa rasilimali hiyo umeendelea kubainika katika nchi mbalimbali zikiwemo nchi
jirani. Masoko tunayotegemea kuuza gesi
yetu ndiyo ambayo yana tegemewa pia na nchi nyingine zenye gesi.
Katika
mazingira ya aina hii ni wazi kwamba tutegemee ushindani
mkubwa wa biashara ya gesi kwa kuzingatia nguvu ya soko ambayo
zinaonesha kwamba kuna uwezekaano uzalishaji wa gesi ukawa mkubwa kuliko
mahitaji (global oversupply of gas
against low demand).
Mheshimiwa
Spika, Hata hivyo, malengo ya Serikali
ya kuanza kuuza gesi nje ya nchi ifikapo mwaka 2023 yanaweza yasifikiwe
kutokana na kasi ndogo ya Serikali katika kukamilisha ujenzi wa mtambo wa
kusindika gesi asilia (LNG plant). Sambamba na hilo
kuwe na mkakati madhubuti kuhusu matumizi ya ndani ya gesi asilia kwa lengo la
kutumia kikamilifu soko la ndani kabla ya kuatafuta soko la nje.
Hata hivyo, kamati
inaipongeza Serikali kwa kuanza kutumia soko la ndani kwa kuwezesha gesi hiyo
kutumika katika mitambo ya Kinyerezi I
ambayo inauwezo wa kuzalisha MW 150.
2.4
Maoni ya Jumla kuhusu Utekelezaji wa Miradi ya
Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2015/2016
Mheshimiwa Spika, kutokana
na ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo Kamati inatoa maoni yafuatayo:-
i)
Serikali iandae Mpango
mkakati utakaowezesha usimamizi na matumizi wa Gesi asilia. Kamati inashangazwa
na Kiwanda cha Dangote kutotumia Gesi inayozalishwa Mtwara.
ii)
Serikali iharakishe ukamilishwaji
wa Mradi wa usindikaji gesi (Liquefied Natuaral Gas) utakaowezesha gesi hiyo
kusafirishwa kwa urahisi.
iii)
Kuwe na usimamizi mzuri
na wa karibu kwa Wakandarasi wanao tekeleza miradi ya maendeleo hususan Miradi
ya REA.
iv)
Serikali itenge fedha
za kutosha na kuzipeleka kwa wakati kwenye miradi ya kimkakati kama vile Mgodi
wa makaa ya Mawe wa Kiwira.
v)
Serikali iwekeze
katika miundombinu na utaalamu wa madini ya vito ili kuwezesha ukataji na
uuzaji wa Tanzanite kufanyika hapa nchini.
vi)
Madeni ya Wakandarasi yalipwe kwa wakati ili kuepusha ongezeko la gharama linalotokana na Serikali kulipa fidia.
vii)
Serikali itatafute namna bora ya kumaliza migogoro ya mrefu ya baina ya
Wawekezaji na Wachimbaji wado wadogo.
3.0
UCHAMBUZI WA TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA BAJETI NA UZINGATIAJAI
WA MAONI YA KAMATI KWA MWAKA WA FEDHA WA
2015/2016
Mheshimiwa
Spika, Kamati ilifanya uchambuzi wa Bajeti kwa kuzingatia mambo makuu matatu ambayo
ni Makusanyo ya Maduhuli kwa mwaka wa
fedha 2015/2016, Hali ya upatikanaji wa fedha kutoka Hazina na Uzingatiaji wa
maoni na ushauri uliotolewa na Kamati ya Nishati na Madini wakati huo.
Mheshimiwa
Spika, naomba kuliarifu
Bunge lako tukufu kuhusu matokeo ya uchambuzi huo kama ifuatavyo:-
3.1 Uchambuzi wa Taarifa
kuhusu Ukusanyaji wa Maduhuli kwa mwaka wa fedha 2015/2016
Mheshimiwa Spika, Wizara ilipanga kukusanya maduhuli jumla ya Shilingi bilioni
291.98 sawa na asilimia 45.5 ya
bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2015/2016. Taarifa ya utekelezaji inaonesha
kuwa, hadi kufikia Machi, 2016, Wizara ilikuwa imekusanya jumla ya shilingi bilioni 157.64 sawa na asilimia 54.99 ya lengo.
Mwenendo huu ni ishara ya kutofanikiwa
kwa lengo la makusanyo ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016. Ni Maoni ya Kamati kwamba, Wizara iweke makadirio
ya makusanyo ambayo ni halisi badala ya kuwa na makadirio makubwa
yasiyotekelezeka.
Mheshimiwa Spika, Kamati imebaini kuwa mchango wa idara ya Madini kwa mwaka
fedha 2016/2017 umeshuka kwa asilimia 19.4 ikilinganishwa na Mwaka 2015/16 wakati mchango wa idara ya Nishati umeongezeka kwa asilimia 25.5 ikilinganishwa
na Mwaka 2015/16.
Ufafanuzi zaidi umeoneshwa kupitia Jedwali Na. 01 la Taarifa hii.
2015/2016
|
2016/2017
|
|||
VYANZO VYA MAPATO
|
KIASI
|
ASILIMIA
|
KIASI
|
ASILIMIA
|
IDARA YA MADINI
|
211,962,385,000
|
72.6
|
215,962,385,000
|
58.3
|
IDARA YA NISHATI
|
79,697,501,000
|
27.3
|
154,377,501,000
|
41.6
|
IDARA NA VITENGO VINGINE
|
324,000,000
|
0.1
|
344,003,000
|
0.1
|
JUMLA KUU
|
291,983,889,000
|
100
|
370,683,889,000
|
100
|
Aidha Kamati ilielezwa sababu zilizosababisha
kushuka kwa makusanyo kwa Mwaka wa Fdha 2015/2016 kama ifuatavyo:-
i)
Kushuka kwa bei ya dhahabu katika Soko la Dunia
ii)
Kupungua kwa uzalishaji katika Migodi; na
iii)
Kupungua kwa shughuli za utafiti katika Sekta za Nishati na Madini;
3.2
Upatikanaji wa Fedha kutoka Hazina
Katika Mwaka wa Fedha 2015/2016 Wizara ya
Nishati na Madini iliidhinishiwa jumla ya shilingi
bilioni 642.12 kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake. Taarifa ya Wizara
inaonesha kuwa, Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 20151/2016 imeongezeka hadi kufikia shilingi
bilioni 762.12 sawa na asilimia 18 ya
bajeti iliyoidhinishwa na Bunge. Ongezeko hili limetokana na uhamisho wa fedha za ndani wa shilingi
bilioni 120 ili kuongeza bajeti ya utekelezaji wa Mradi wa KInyerezi II MW 240
na ulipaji wa sehemu ya madeni ya Ankara za umeme yanayodaiwa na TANESCO na Taasisi
za Serikali.
Mheshimiwa Spika, Kamati inapongeza jitihada za Serikali kwa nia yake ya dhati ya
kuanza kutekeleza Mradi huu Muhimu ambao
utaweza kuzalisha umeme wa MW 240, ongezeko hili la MW 240 katika Grid ya Taifa
itasaidia kupunguza tatizo la upatikanaji wa umeme katika maeneo mbali mbali ya
nchi hii na kuwaletea wananchi maendeleo
yanayokusudiwa hasa maendeleo ya Viwanda.
Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia mwezi Machi, 2016 Wizara ilikuwa imepokea jumla ya shilingi bilioni 625.34 sawa na asilimia themanini na mbili 82. Kati ya fedha
hizo shilingi
bilioni 579.54 zilikuwa ni fedha za
Miradi ya Maendeleo sawa na asilimia
tisini na tatu 93 ya fedha zilizopatikana hadi kufikia Machi, 2016. Katika fedha hizo shilingi bilioni 546.18 sawa na asilimia tisini na nne nukta
mbili 94.2 ni fedha za ndani na shilingi bilioni 33.36 sawa na asilimia tano nukta nane 5.8
ni fedha za nje.
Mheshimiwa Spika, ili kutoa picha halisi ya uwiano kati ya Bajeti iliyoidhinishwa na fedha
zilizopatikana.
Jedwali Na. 2 la tarifa hii linafafanua
BAJETI ILIYOIDHINISHWA 2015/2016
|
FEDHA ILIYOPATIKANA HADI MACHI,2016
|
|||
UFAFANUZI
|
KIASI
|
ASILIMIA
|
KIASI
|
ASILIMIA
|
JUMLA KUU
|
642.12
|
100
|
625.34
|
97.4
|
FEDHA ZA MAENDELEO
|
502.3
|
78.2
|
579.54
|
115.4
|
MATUMIZI YA KAWAIDA
|
139.82
|
21.7
|
45.8
|
33
|
CHANZO: Taarifa ya Wizara ya Nishati na Madini fungu 58 kuhusu utekelezaji wa bajeti kwa
mwaka wa fedha 2015/2016.
Mheshimiwa Spika, Kamati
imefanya upembuzi yakinifu wa hali ya upatikanaji wa fedha unaonesha kuwa
Wizara ilipata fedha za kugharamia miradi ya maendeleo kwa kiasi kinachozidi
Bajeti iliyoidhinishwa na Bunge lako
tukufu kwa mwaka wa fedha 2015/2016, kama inavyofafanuliwa katika Jedwali namba mbili la tarifa hii.
Mheshiiwa Spika, Kutokana na ongezeko hilo, Kamati ilitaka kupata
maelezo ya kina ili kulinganisha upatikanaji wa fedha na bajeti iliyoidhinishwa.
Aidha,
ni maoni ya kamati kuwa ili kuwe na
utekelezaji bora wa Bajeti, Wizara inapaswa kuzingatia mahitaji halisi,
vipaumbele na uwezekano wa upatikanaji wa fedha kwa kufanya hivyo, itakuwa si
rahisi upatikanaji wa fedha kuzidi kiasi
cha Bajeti inayoidhinishwa na Bunge.
3.3
Mapitio ya Utekelezaji wa Ushauri wa Kamati
Mheshimiwa Spika, wakati wa kuchambua Bajeti ya Wizara
kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016, Kamati ilitoa Maoni, Ushauri na Mapendekezo
katika maeneo ya Umeme, Gesi asilia,
Biashara ya Mafuta, Utendaji wa Wizara na Taasisi chini ya Wizara. Napenda
kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa baadhi ya Ushauri uliotolewa na Kamati
haukuzingatiwa na kufanyiwa kazi na Serikali kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, bado kuna tatizo la kukaimisha Watendaji Wasaidizi kwa
muda mrefu bila kuwapatia mamlaka kamili ya kiutendaji. Tatizo hili lipo
STAMICO na Chuo cha Madini. Hali hii inaendelea kukwamisha utekelezaji bora wa
Mipango ya Maendeleo. Aidha, jitihada za Serikali za kutafutia ufumbuzi suala
hili siyo za kuridhisha sana.
Mheshimiwa Spika, Hatua zilizochukuliwa na Serikali kuhusu utekelezaji wa
miradi ya umeme wa jua (Solar Energy), umeme wa upepo (Wind Energy), umeme wa joto
ardhi (Geothermal) na Tungamotaka (Renewable Energy) haioneshi nia ya dhati ya
Serikali ya kutekeleza miradi hiyo muhimu hasa kwa kutengewa bajeti kidogo mwaka 2016/17.
Mheshimiwa Spika, Kamati haikuridhishwa na kasi ya EWURA katika kuwaelimisha
na kuwasimamia wajenzi na wamiliki wa vituo vya mafuta hasa katika maeneo ya Vijijini,
Kanuni zilizo andaliwa kuhusu
Usimamizi wa Ujenzi na Uendeshaji wa Vituo maeneo ya vijijini (The Petroleum (Rural Retail Outlets
Operation) Rules, 2015, Kanuni hizi hazifahamiki kwa watumiaji hivyo kuleta
usumbufu wakati wa ukaguzi wa vituo kwa kutoza faini ya Shilingi milioni tano
hata kama wana vibali vya ujenzi toka Halmashauri na NEMC.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na utaratibu mzuri wa fedha za REA uliwekwa
kisheria kuhusu fedha zake kulindwa (Ring Fenced) bado upatikanaji wake
hauridhishi, Miradi ya REA kwa mwaka uliopita 2015/2016 ulitengewa Shilingi 357.1 na hadi sasa zimepelekwa
Shilingi bilioni 168 sawa na
asilimia arobaini na saba (47%) ya bajeti yote iliyokuwa imetengwa katika
miradi hiyo.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kulipa madeni ya TANESCO kupitia
Hazina na kwa mwaka 2015/2016 zimelipwa jumla ya Shilingi bilioni 184 ambayo ni sawa na asilimia 59.74 ikiwa ni madeni ya Serikali na Taasisi zake, utaratibu huu
wa malipo unakwamisha utekelezaji shughuli mbali mbali za TANESCO.
Aidha, Serikali imeendelea kutekeleza
maoni na ushauri wa Kamati kwa kuingiza kwenye Bajeti ya Wizara ya mwaka
2016/17, hivyo utekelezaji unaendelea.
4.0
UCHAMBUZI WA MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA
MATUMIZI KWA
(FUNGU 58) MWAKA WA FEDHA 2016/2017
4.1
Mapitio ya Malengo ya Wizara kwa mwaka wa fedha
2016/2017
Mheshimiwa
Spika, Kwa mwaka wa fedha
2016/2017 wizara imejiwekea Malengo Makuu Matano (5) yafuatayo:-
i)
Kuimarisha
usimamizi na uendelezaji wa Sekta ya Nishati kwa maendeleo endelevu ya Taifa.
ii)
Kuboresha
uendelezaji na usimamizi endelevu wa rasilimali za madini kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi
iii)
Kuimarisha
utoaji wa huduma kwa wadau katika Sekta za Nishati na Madini.
iv) Kuboresha utoaji wa huduma kwa watumishi
waathirika wa VVU na UKIMWI ili kupunguza maambukizi
v)
Kuondoa
vitendo vya Rushwa katika sekta ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa
Spika, Kamati ilibaini
kuwa
Wizara ya Nishati na Madini imekuwa na malengo haya ya muda mrefu kuanzia mwaka
2011/12 hadi mwaka 2016/17. Kamati
ilitaka kujiridhisha kuhusu kujirudia kwa malengo hayo na kufanya rejea katika
Hati Idhini (Government Instrument) iliyochapishwa katika Gazeti la Serikali Na. 144 la tarehe 22 Aprili, 2016. Kamati ilibaini kuwa malengo hayo yanaendana
na Mpango wa Taifa, aidha Kamati katika uchambuzi wa bajeti imeridhia malengo
hayo kutokana na umuhimu wake.
Mheshimiwa
Spika, malengo haya
yamezingatia majukumu yaliyoainishwa kwa mujibu wa Sheria ya Utekelezaji wa
Majukumu ya Wizara, sura 299, The Ministers
(Discharge of the Ministerial Functions) Act.
4.2
Uchambuzi wa Makadirio ya Mapato
Mheshimiwa
Spika, Makisio ya
makusanyo ya Maduhuli kwa Mwaka wa Fedha 2016/17 yanakadiriwa kuwa jumla ya Shilingi 370.68 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 286.66 kwa mwaka wa
fedha 2015/16. Kati ya makusanyo hayo Shilingi bilioni 215.96 sawa na asilimia 58.3 zitakusanywa
na idara ya Madini, shilingi 154.378
sawa na asilimia 41.6 zitakusanywa na idara ya Nishati na shilingi 344,003,000 sawa na asilimia 0.1 zitakusanywa na idara na
vitengo vingine katika Wizara.
Makadirio ya makusanyo ya mapato yameongezeka kwa
asilimia 29.3 ikilinganishwa na makadirio
ya makusanyo ya mwaka 2015/16. Aidha ongezeko hili la Makusanyo ya maduhuli kwa
mwaka wa fedha 2016/17 linatokana na sababu zifuatazo:-
i)
Kuendelea
kutumia Gesi Asilia badala ya mafuta mazito katika miradi mikubwa ya uzalishaji
umeme;
ii)
Kuendelea
kuhamasisha shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia ili kuongeza uzalishaji
na mauzo;
iii)
Kuendeleza
kuimarisha usimamizi wa wachimbaji
wadogo kwa kutoa huduma za ugani na kuwapa mafunzo ili wafuate Sheria katika
shughuli zao ikiwa ni pamoja na kulipa Maduhuli ya Serikali;
iv) Wizara kutoa malengo ya ukusanyaji kwa kila
Kamishna Msaidizi na Mkazi katika ofisi za Mikaoni;
v)
Kuimarisha
ushirikiano na Taasisi nyingine za Serikali katika kuzuia utoroshaji na
biashara isiyo rasmi ya madini ikiwa ni pamoja na kuanzisha masoko ya madini ya
vito;
vi) Kukuza matumizi ya ndani ya gesi asilia ili
kuongeza mapato na kupunguza uharibufu wa mazingira unaotokana na matumizi ya
kuni na mkaa.
4.3
Uchambuzi wa Makadirio ya Matumizi
Mheshimiwa
Spika, makadirio ya
matumizi ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka 2016/2017 ni jumla
ya Shilingi 1,122,845,741,000
ikilinganishwa na Shilingi 642,123,079,000 zilizoidhinishwa na Bunge kwa mwaka
2015/2016, hii ni sawa na ongezeko la asilimia
sabini na nne nukta tisa 74.9. Kamati ilielezwa kuwa ongezeko hili linatokana
na kuongezeka kwa fedha za miradi ya Maendeleo.
Aidha, Bajeti ya
fedha za ndani za REA imeongezeka kutoka Shilingi 357,117,000,000 mwaka 2015/16 hadi Shilingi 534,400,000,000 kwa mwaka 2016/17, sawa na ongezeko la asilimia arobaini na tisa nukta sita 49.6
ya bajeti ya REA kwa mwaka wa fedha 2015/2016.
Mheshimiwa
Spika, Bajeti ya miradi
ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2016/2017 inakadiriwa kuwa jumla ya Shilingi
1,056,354,669,000 ikilinganishwa na Shilingi
502,303,938,000 kwa mwaka 2015/16, ongezeko hilo ni sawa na asilimia mia moja na kumi nukta tatu 110.3.
Ongezeko hilo la Bajeti ya Maendeleo ni sawa na asilimia tisini na nne 94
ya Bajeti yote ya Wizara.
Mheshimiwa
Spika, fungu 58 kwa mwaka 2016/2017 fedha za ndani za maendeleo zimeongezeka
kutoka shilingi bilioni 280.00 hadi shilingi bilioni 724.84, fedha za nje
zimeongezeka kutoka shilingi bilioni
85.35 hadi shilingi bilioni 331.51.
Aidha, bajeti ya matumizi ya kawaida kwa mwaka wa
fedha 2016/17 imetengwa jumla ya Shilingi
66,481,072,000 sawa na asilimia sita
6 ya bajeti yote ya Wizara kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 38,654,138,000 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC)
na shilingi bilioni 27.83 ni kwa ajili ya mishahara ya Watumishi
wa Wizara na Taasisi zake.
Bajeti ya matumizi ya kawaida imepungua kwa kiasi
kikubwa sana ukilinganisha na bajeti ya mwaka wa Fedha 2015/16 ambapo ilikuwa
shilingi 171,613,498,000 sawa na asilimia thelathini na mbili 32 ya Bajeti yote
ya Wizara, bajeti hii ni pungufu kwa asilimia
38.73 ya bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016.
Mheshimiwa
Spika, Bajeti ya Miradi ya
Maendeleo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 ni sawa na asilimia 10.04 ya Bajeti Kuu ya Maendeleo ya Taifa. Bajeti ya Matumizi mengineyo ni sawa na asilimia 0.49 ya Bajeti ya Matumizi ya
kawaida ya Taifa, bajeti hii ni pungufu ya bajeti ya mwaka 2015/2016 kwa asilimilia 1.28.
Mheshimiwa
Spika, mwaka wa fedha
2016/17 bajeti ya Miradi ya maendeleo
imeongeza kwa asilimaia 110.3 toka kwenye Bajeti ya Miradi ya Maendeleo kwa Mwaka
wa Fedha 2015/2016. Ongezeko hilo litasaidia
kukamilisha miradi kipumbele ya Taifa hasa kwa upande wa Nishati na miradi
ya kimkakati kwa Wizara itatekelezwa kwa ufanisi.
5.0
MAONI NA USHAURI WA KAMATI
Mheshimiwa Spika, Kamati katika kutekeleza
majukumu yake ya kikanuni ya ukaguzi wa miradi, uchambuzi wa Taarifa ya Utekelezaji
wa Bajeti ya Wizara kwa Mwaka wa fedha 2015/16 na uchambuzi wa makadirio na
matumizi ya Wizara kwa mwaka wa Fedha 2016/17 ufuatao ni ushauri na maoni ya
Kamati:-
i) Serikali
iandae Mpango mkakati utakaowezesha usimamizi mzuri wa Gesi asilia
inayozalishwa nchini ikiwa ni pamoja na kutafuta masoko.
ii) Serikali
iharakishe ukamilishwaji wa Mradi wa usindikaji gesi (Liquefied Natuaral Gas)
utakaowezesha gesi hiyo kusafirishwa kwa urahisi
iii) Kuwe
na usimamizi mzuri na wa karibu kwa Wakandarasi wanao tekeleza miradi ya
maendeleo hususan Miradi ya REA.
iv) Serikali
itenge fedha za kutosha na kuzipeleka kwa wakati kwenye miradi ya kimkakati
kama vile Mgodi wa makaa ya Mawe wa Kiwira.
v) Serikali
iwekeze katika miundombinu na utaalamu wa madini ya vito ili kuwezesha ukataji
na uuzaji wa Tanzanite kufanyika hapa nchini.
vi) Madeni ya Wakandarasi
yalipwe kwa wakati ili kuepusha ongezeko la gharama linalotokana na Serikali
kulipa fidia.
vii) Serikali itekeleze kwa dhati ushauri na
mapendekezo ya Tume mbalimbali zilizoundwa ili kutua mgogoro wa muda mrefu wa
Wachimbaji wadogo wadogo wa Tanzanite.
viii) Chuo
cha Madini kitengewe fedha za kutosha ili kuweza kuzalisha wataalamu watakaoendeleza
rasilimali muhimu za Taifa hili.
ix) Wakandarasi
wanaotekeleza miradi mbali mbali walipwe kwa wakati ili kukwepa kulipa fidia
zisizo za lazima.
x)
Fedha za REA zinazokusanywa kutoka kwenye tozo
ziwasilishwe moja kwa moja kwenye Mfuko wa Nishati Vijijini .
xi)
Serikali
isimamie kwa makini ukamilishwaji wa
miradi ya vipaumbele ya kuzalisha umeme ili kuwezesha upatikanaji wa umeme wa
kutosha na wa uhakika na kwa bei nafuu.
xii)Kamati inaitaka Serikali kuchukua hatua madhubuti na
zakupimika katika kusimamia madini haya adimu ya Tazanite ili kuiondoa nchi
katika aibu ya utoroshaji wa Madini.
6.0
HITIMISHO
Mheshimiwa
Spika, nichukue fursa hii
kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge, kwa kazi nzuri
mnayoifanya ya kuliongoza Bunge. Mungu awajalie afya njema, hekima na busara
katika kutekeleza wajibu huu mkubwa tuliowakabidhi.
Kwa namna ya pekee nawashukuru Wajumbe wa Kamati
kwa ushirikiano walionipa wakati wa kujadili na kuchambua makadirio ya Mapato
na Matumizi ya fungu 58 kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
Naomba
majina yao yaingizwe kwenye Hansard kama yalivyo:-
1. Mhe. Doto Mashaka Biteko, Mb - Mwenyekiti
2. Mhe. Deogratius Ngalawa, Mb - M/Mwenyekiti
3. Mhe. Mohamed Juma Khatib, Mb - Mjumbe
4. Mhe. Ally Mohamed Keissy, Mb - “
5. Mhe. Yussuf Kaiza Makame, Mb - “
6. Mhe. Zainabu Mussa Bakar, Mb - “
7. Mhe. Haroon Mulla Pirmohamed,
Mb - “
8. Mhe. Mwantakaje Haji Juma, Mb
- “
9. Mhe. Daimu lddi Mpakate, Mb - “
10. Mhe. Catherine Valentine Magige, Mb - “
11. Mhe. Oscar Rwegasira Mukasa, Mb - “
12. Mhe. Stella Ikupa Alex, Mb - “
13. Mhe. Joyce Bitta Sokombi, Mb - “
14. Mhe. Bahati Ali Abeid, Mb - “
15. Mhe. Mauled Said Abdalah Mtulia,
Mb - “
16. Mhe. Desderius John Mipata,
Mb - “
17. Mhe. Katani Ahmad Katani, Mb - “
18. Mhe. Susan Limbweni
Kiwanga,Mb - “
19. Mhe. Vedastus Mathayo
Manyinyi, Mb - “
20. Mhe. Bupe Nelson Mwakang’ata,
Mb - “
21. Mhe. Maryam Salum Msabaha, Mb
- “
22. Mhe. Innocent Lugha Bashungwa,Mb
- “
23. Mhe. Ezekiel Magolyo Maige,
Mb - “
24. Mhe. Wilfred Muganyizi
Lwakatare, Mb - “
25. Mhe. Dunstan Luka Kitandula,
Mb - “
Mheshimiwa
Spika, nachukua fursa hii
pia kumshukuru Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Didimu Kashilillah, Mkurugenzi wa
Idara ya Kamati za Bunge Ndg. Athuman Hussein, Makatibu wa Kamati Ndg. Mwanahamisi
Munkunda na Ndg. Felister Mgonja, kwa kuratibu shughuli zote za Kamati na
hatimaye kukamilisha Taarifa hii kwa wakati. Aidha, nawashukuru Watendaji wote wa Ofisi ya
Bunge kwa ushirikiano wao ulioiwezesha Kamati kutekeleza majukumu yake kwa
ukamilifu.
Mheshimiwa
Spika, naomba sasa Bunge
lako Tukufu likubali kuidhinisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fungu 58 kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
ambayo ni Shilingi 1,122,845,741,000.
Mheshimiwa
Spika, Naunga mkono hoja
na Naomba
kuwasilisha.
Dotto Mashaka Biteko, (Mb)
MWENYEKITI
KAMATI YA BUNGE YA NISHATI NA
MADINI
20 May, 2016
Umetisha mkuu. Kazi nzuri.
ReplyDelete